Genesis 21

Kuzaliwa Kwa Isaka

1 aWakati huu Bwana akamrehemu Sara kama alivyokuwa amesema, naye Bwana akamtendea Sara kile alichokuwa ameahidi. 2 bSara akapata mimba, akamzalia Ibrahimu mwana katika uzee wake, majira yale ya Mungu aliomwahidi. 3 cIbrahimu akamwita Isaka yule mwana ambaye Sara alimzalia. 4 dIsaka alipokuwa na umri wa siku nane, Ibrahimu akamtahiri, kama Mungu alivyomwamuru. 5 eIbrahimu alikuwa na miaka 100 wakati Isaka mwanawe alipozaliwa.

6 fSara akasema, “Mungu ameniletea kicheko, kila mmoja atakayesikia jambo hili atacheka pamoja nami.” 7 gAkaongeza kusema, “Nani angemwambia Ibrahimu kuwa Sara angenyonyesha watoto? Tena nimemzalia mwana katika uzee wake.”

Hagari Na Ishmaeli Wafukuzwa

8 hMtoto akakua, akaachishwa kunyonya. Siku hiyo Isaka alipoachishwa kunyonya, Ibrahimu alifanya sherehe kubwa. 9 iLakini Sara aliona kuwa mwana ambaye Hagari, Mmisri, aliyemzalia Ibrahimu alikuwa anadhihaki, 10 jSara akamwambia Ibrahimu, “Mwondoe mwanamke huyo mtumwa pamoja na mwanawe, kwa kuwa mwana wa mwanamke mtumwa kamwe hatarithi pamoja na mwanangu Isaka.”

11 kJambo hili lilimhuzunisha sana Ibrahimu kwa sababu lilimhusu mwanawe. 12 lLakini Mungu akamwambia, “Usihuzunike hivyo kwa sababu ya kijana na mtumishi wako wa kike. Sikiliza lolote Sara analokuambia, kwa sababu uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaka. 13 mNitamfanya huyu mwana wa mtumishi wako wa kike kuwa taifa pia, kwa sababu naye ni uzao wako.”

14 nKesho yake asubuhi na mapema, Ibrahimu akachukua chakula na kiriba cha maji, akampa Hagari. Akaviweka mabegani mwa Hagari, akamwondoa pamoja na kijana. Hagari akashika njia, akatangatanga katika jangwa la Beer-Sheba.

15Maji yalipokwisha kwenye kiriba, akamwacha kijana chini ya mojawapo ya vichaka. 16 oKisha akajiendea zake akaketi karibu, umbali wa kutupa mshale, akawaza, “Siwezi kumwangalia kijana akifa.” Ikawa alipokuwa ameketi pale karibu, akaanza kulia kwa huzuni.

17 pMungu akamsikia kijana akilia, malaika wa Mungu akamwita Hagari kutoka mbinguni na kumwambia, “Kuna nini Hagari? Usiogope, Mungu amesikia kijana analia akiwa amelala pale. 18Mwinue kijana na umshike mkono, kwa maana nitamfanya kuwa taifa kubwa.”

19 qNdipo Mungu akamfumbua Hagari macho yake naye akaona kisima cha maji. Hivyo akaenda akajaza kiriba maji na kumpa kijana anywe.

20 rMungu akawa pamoja na huyu kijana alipokuwa akiendelea kukua. Aliishi jangwani na akawa mpiga upinde. 21 sAlipokuwa akiishi katika Jangwa la Parani, mama yake akampatia mke kutoka Misri.

Mapatano Katika Beer-Sheba

22 tWakati huo Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakamwambia Ibrahimu, “Mungu yu pamoja nawe katika kila kitu unachofanya. 23 uSasa niapie hapa mbele za Mungu kwamba hutanitenda hila mimi, watoto wangu wala wazao wangu. Nitendee mimi na nchi ambayo unaishi kama mgeni wema ule ule ambao nimekutendea.”

24Ibrahimu akasema, “Ninaapa hivyo.”

25 vNdipo Ibrahimu akalalamika kwa Abimeleki kuhusu kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki walikuwa wamekinyang’anya. 26Lakini Abimeleki akasema, “Sijui ni nani ambaye amefanya hili. Hukuniambia, leo tu ndipo ninasikia habari zake.”

27 wHivyo Ibrahimu akaleta kondoo na ng’ombe akampa Abimeleki, nao watu hawa wawili wakafanya mapatano. 28Ibrahimu akatenga kondoo wa kike saba kutoka kwenye kundi, 29Abimeleki akamuuliza Ibrahimu, “Ni nini maana ya hawa kondoo wa kike saba uliowatenga peke yao?”

30 xIbrahimu akamjibu, “Upokee hawa kondoo wa kike saba kutoka mkononi mwangu kama ushahidi kuwa nilichimba kisima hiki.”

31Hivyo mahali pale pakaitwa Beer-Sheba, kwa sababu watu wawili waliapiana hapo.

32 yBaada ya mapatano kufanyika huko Beer-Sheba, Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakarudi katika nchi ya Wafilisti. 33 zIbrahimu akapanda mti wa mkwaju huko Beer-Sheba, na hapo akaliitia jina la Bwana Mwenyezi Mungu wa Milele. 34 aaNaye Ibrahimu akakaa katika nchi ya Wafilisti kwa muda mrefu.
Copyright information for SwhKC